TUTAKAPOKUWA tunaazimisha miaka yetu 50 ya Uhuru kwa mambo na vijambo visivyo tofauti na wale waliokwishatutangulia kuadhimisha miaka yao 50 kubwa litakalojitokeza ni Tanzania kushindwa kujifunza toka nchi za Kiarabu, Korea zote mbili, China, India, Japani, Norway, Vietnam, Cambodia, Indonesia, Malaysia na nchi nyingine kama hizo kwamba hatua ya kwanza kwa nchi yoyote kuendelea ni kutumia lugha yake mama na sio kutumia lugha za kigeni katika kufundishia.
Tumewaona wanaopigania Kiingereza kuendelea kutumika wao wenyewe wakishindwa kujieleza vizuri katika lugha zote mbili kwa kuwa hakuna misingi madhubuti iliyoweka ya kujifunza na kuitawala lugha yetu au ya Kiingereza au nyingine iwayo.
Wanaopeleka watoto wao nje wanarudi na Kiingereza cha puani na mitindo ya Kizungu au KImarekani na mara nyingi wanajikuta wakiwa kivutio cha ajabu na mshangao kwa wanaowazunguka sio kwa sababu wanaona wana akili, busara na hekima lakini kwa jinsi walivyoweza kuwa nyani wazuri katika kumuiga binadamu mzungu.
Wakati ambapo wazazi wengi wenye uwezo wanajiuliza kama wawapeleke watoto wao magharibi au mashariki au katikati ya dunia wengi wanaweweseka na kutokuamini kwamba China au Korea au Japani au Imarati siku moja ndiyo zitakuwa nchi tajiri na bora kuliko Marekani na Uingereza. Hawajaamini kutokana na mazoea na kasumba za kikoloni zilizowageuza mateja na watoto wao wanasesere wa hata michezo ya timu za Uingereza na Marekani bila kujua wanachokipata ni nini. Lakini haya pengine ni matokeo ya nchi kuwa nyuma kimaendeleo hata katika michezo na kukosa timu hata kama Mazembe tu ya kuishangilia na kujivunia tunaishia kugombana kuhusu Mancheseter United, Chelsea, Arsenal na kadri tunavyochelewa kukikubali Kiswahili itatuchukua miaka kadhaa hata mwenetu kuchezea timu kama hizo.
Labda Mzee Bakhresa atatutoa toka aibu hii kupitia Azam F.C. na Academy yake na sisi tunampa chalenji kwanini asigeuze chuo chake kiwe ni Chuo Kikuu kinachofundisha kila kitu kwa Kiswahili? Na kisha pembeni aanzishe maabara za kujifunza lugha kama vile Kiarabu, Kifaransa, KIhispania, Kichina, Kijapani, Kireno na kadhalika ili wachezaji wake waweze kuwa wanaongea lugha mbili au tatu na kuwacheka hao wanaong'ang'ania kufundisha kwa Kiingereza ili mtoto aelewe Kiingereza na bado kinamshinda kwa sababu kinachohitajika ni maabara na elimu kwa vitendo na sio hicho wanachokifanya ?
MAANA, sisi wanaharakati wa Kiswahili tunachokisema ndio hiki na sio kingine. Yaani, tufundishe kwa Kiswahili toka chekechea hadi Chuo Kikuu, lakini kila chekechea, kila shule ya msingi, sekondari na Chuo Kikuu sambamba na elimu hiyo ya Kiswahili inakuwa na MAABARA YA LUGHA ambako mtoto atachagua lugha mbili au tatu za kigeni kujifunza kwa miaka yake yote atakayokuwa shuleni hadi ahitimu tuone kama hatutaionesha Afrika kama sio dunia maajabu! Inshallah!
Kwanini basi katika kuadhimisha miaka 50 ya Uhuru na katika kuandika katiba mpya suala hili la matumizi ya lugha ya Kiswahili kwa utaratibu uliooneshwa hapo juu lisiwe suala litakaloamua mustakabali wetu na maendeleo ya elimu inayoweza kuwashirikisha watu wote Tanzania?
KISWAHILI-LUGHA YATIMA YA AFRIKA
Tunatwanga kuelekea KISWAHILI2UNIVERSITY na zisipokoboleka na kusagika vizuri watoto na wajukuu watamalizia. Kazi kwetu kuanza, na kuanza tunaamini ni ushujaa!
Monday, May 23, 2011
KINACHOKUJA: ISTILAHI YA MISINGI YA MENEJIMENTI
HIVI sasa tunaandaa istilahi kwa ajili ya somo la Misingi ya Menejimeni kwa Kiswahili. Tunaomba ushirikiano wako katika kuipitia Istilahi hizo na kutupa mrejesho kwa wakati muafaka ili tuweze kushirikisha mawazo yenu na kupata kilicho bora katika hatua hizi za mwanzo ambapo hakuna anayetujua, anayetuona, anayetusikia wala anayeamini kwamba tumeanza jambo la kihistoria katika maendeleo ya nchi yetu. Yaani, kujijenga kama nchi kwa kutumia maziwa yake yenyewe badala ya yale ya wageni.
Subscribe to:
Posts (Atom)